KAMATI NNE ZA BUNGE ZAKUTANA KUJADILI MGONGANO WA SHERIA NA KANUNI KATIKA SEKTA YA MALIASILI, ARDHI, MIFUGO NA MADINI, PAMOJA NA MAZINGIRA WEZESHI YA SEKTA YA UTALII NCHINI

Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) kwa kushirikiana wadau wake Ujamaa Community Resource Team (UCRT), Tanzania Tour Operators (TATO),  Tanzania Confederation of Tourism (TCT), Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) na Mazingira Network Tanzania (MANET) wamepata fursa ya kukutana na wajumbe zaidi ya 90 kutoka Kamati ya Ardhi, Maliasili na UtaliiNishati na MadiniKilimo, Mifugo na Maji na Kamati ya Sheria Ndogo

Mkutano huu pia ulihudhuriwa Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia uwekezaji Mh. Angela Kairuki;Waziri wa madini Mh. Dotto Biteko; Naibu waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mh Angelina Mabula, Naibu waziri wa maliasili na utalii Mh. Costantine Kanyasu, Naibu waziri wa viwanda na biashara. Wengine walikuwa ni Kamishna wa Ardhi,  pamoja ya wataalamu kutoka katika wizara hizi.

Malengo ya mkutano huu ilikuwa kupata mtazamo wa wabunge wajumbe wa kamati mbalimbali zinazogusa moja kwa moja maswala ya rasilimali asili ikiwemo wanyamapori, kujua ukubwa wa tatizo na kukubaliana namna bora ya kushirikiana kwa sekta hizi kutatua maswala ya mwingiliano wa sheria hizi.

Mjadala wa Wajumbe wa Kamati na Mawaziri kutoka kwenye Wizara husika ulijikita zaidi kwenye mgongano uliopo katika sheria na kanuni mbalimbali kwa sekta hizi, madhara yake na mapendekezo ya kuboresha sheria hizi.  Wabunge walijadili kwa kirefu Sheria ya Ardhi namba 4 ya 1999, Sheria ya Ardhi ya vijiji namba 5 ya 1999, Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, Kanuni za ushoroba na mapito ya wanyama ya 2018 na Sheria ya nyanda za malisho ya mwaka 2010. Ambazo kwa namna moja ama nyingine mwingiliano wake unaathiri utendaji kisekta na hasa sekta ya Maliasili na Uhifadhi Wanyamapori na ukosefu wa mazingira wezeshi ya biashara ya utalii na uwekezaji nchini.

Wajumbe kwa pamoja walikubali kwamba upo mgongano kwa sheria mbalimbali, kuipokea hoja iliyowasilishwa, kuahidi kuifanyia kazi kwa muda mfupi na kwa kupitia Ofisi ya waziri Mkuu Uwekezaji Waziri Angela Kairuki  aliahidi kuleta mrejesho kwa mwenyekiti wa mkutano huu Mh Mahmoud Mgimwa kuhusu namna bora ya kufanya iki kuondoa mwingiliano wa kisheria uliopo ili kuleta tija kiuwekezaji na kukuza biashara ya utalii nchini.

Kama mkakati wa kufuatilia ahadi ya waziri: Mwenyekiti wa TAPAFE Mh. Jitu Soni pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kushirikiana na TNRF watafanya mawasiliano na Mheshimiwa Waziri na kisha kutoa mrejesho wa yatakayoamriwa kwa ajili ya mipango ya baadaye.

Relevance: 
Undefined