SHUGHULI ZA UTALII TANZANIA KUANZA TENA.

utalii_tz.png

Utalii tena
Media Folder: 

Tanzania inategemea kuanza kupokea watalii kutokana na kuwepo dalili  kwa  baadhi  ya  nchi  kuruhusu   raia  wake kusafiri  nje  ya  nchi.  Kadhalika  mashirika  kadhaa  ya  ndege  kupanga  kuanza tena  kufanya   ziara  za  kimataifa,   na  baadhi  yao  wataanza   safari  mwishoni  mwa mwezi huu. Tarehe 18 Mei, 2020 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, ametoa mwongozo kuhusu kuendelea kwa shughuli za utalii nchini katika kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID -19.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini, Dkt. Kigwangalla amesema shughuli za Utalii zitaanza tena rasmi huku akisisitiza kuwa, Tanzania itafuata utaratibu wa kujikinga na kuwakinga watalii dhidi ya ugonjwa wa COVID - 19 kwa kufuata na kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Akisisitiza zaidi, Waziri Kigwangalla amesema "Jukumu letu la kwanza tunalinda afya za watanzania na kuwalinda watalii wasipate virusi vya CORONA hadi pale watakapoondoka nchini."

Dkt. Kigwangalla amesema, watalii watakaokuja hapa nchini watakuwa salama kiafya kwani watakuwa tayari wamepimwa katika vituo vya afya vinavyoaminika kabla ya kuanza safari. Serikali itahakikisha watoa huduma walioko kwenye mnyororo wa Utalii kuanzia katika viwanja vya ndege, hotelini na kote wanakohudumia watalii, wanazingatia taratibu za kiafya ili kuwalinda watalii wanaokuja hapa Tanzania dhidi ya virusi vya CORONA.

Waziri Kigwangalla amefafanua kuwa, wahudumu wote walioko kwenye mnyororo wa Utalii, watakuwa wanapimwa mara kwa mara pale wanapojichanganya na watu wengine ili kuhakikisha hawana virusi vya CORONA.

Waziri Kigwangalla amemshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kufungua tena anga la Tanzania na kuondoa sharti la watalii kukaa kwenye karantini kwa siku 14 wanapoingia nchini.

Relevance: 
Undefined