HOTUBA YA MGENI RASMI MHESHIMIWA SULEIMAN JAFFO (MB) NAIBU WAZIRI WA NCHI OR-TAMISEMI KATIKA UZINDUZI WA MRADI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI (DECENTRALISED CLIMATE FINANCE IN TANZANIA) KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA HAZINA NDOGO

  • Waheshimiwa wenyeviti wa Kamati za kudumu za Bunge (Viwanda Biashara na Mazingira na Kamati ya  Bajeti
  • Waheshimiwa wabunge wa majimbo ya Longido, Monduli na Ngorongoro
  •  Makatibu Wakuu kutoka OR – TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Fedha na Mipango,
  • Wawakilishi kutoka Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNCDF)
  • Wawakilishi wa kutoka Taasisi ya  Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED),
  • Wawakilishi kutoka mashirika yasiyo kuwa ya Kiserikali
  • Makatibu Tawala wa Mikoa (Arusha na Dodoma)
  • Wakurugenzi kutoka OR – TAMISEMI
  • Mwenyekiti wa Bodi Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Dodoma
  • Mkuu wa Chuo na wawakilishi kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Dodoma
  • Mkuu wa Chuo na wawakilishi toka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo
  • Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmshauri ( Longido, Monduli na Ngorongoro
  • Wakurugenzi wa Halmashauri (Longido, Monduli na Ngorongoro)
  • Watumishi wengine wa Serikali mlioko hapa leo
  • Wageni  wote  waalikwa
  • Wanahabari,
  • Mabibi na Mabwana.

Habari za Asubuhi

Bwana Yesu Asifiwe

Asalaam Aleykum

Ndugu wageni waalikwa,  

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha leo kufika hapa kwa ajili ya tukio hili muhimu.

Pili naomba nitumie fursa hii kuwakaribisha ninyi nyote katika mji wetu wa Dodoma. Dodoma ni makao makuu ya nchi yetu na mahali muhimu kwa kuwa Bunge letu la Tanzania linafanya shughuli zake za kitaifa hapa. Ni imani yangu kuwa mtatumia muda wenu baada ya mkutano huu kutembelea maeneo muhimu ya Dodoma kama vile Ofisi za Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, na Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho ni kikubwa kuliko vyuo vyote kusini mwa Afrika.

Tatu, niwakaribishe ninyi wote katika mkutano huu wa siku moja wa uzinduzi rasmi wa Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi Tanzania (Decentralised Climate Finance in Tanzania). Mradi huu ni wa ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi ya kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED), Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNCDF LoCAL), mashirika mawili yasiyokuwa ya kiserikali yaani Haki Kazi Catalyst (HKC) na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF).  Ili kuhakikisha uendelevu wa mradi huu hasa katika kupanuka katika maeneo mengine ya Nchi yetu, Taasisi nyingine hususani Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) na Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), zitashiriki katika mradi huu kwa kuzijengea  uwezo Halmashauri zetu katika kuandaa mipango inayozingatia umuhimu wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Ni jambo lililo wazi kwamba, mradi huu umekuja katika wakati muhimu ambapo nchi yetu ya Tanzania na mataifa yote duniani yanazungumza na kuweka mikakati muhimu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Ndugu wageni waalikwa,

Kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi sasa ni tatizo kubwa na tayari tumeanza kupata madhara makubwa katika maisha ya binadamu na pia kwa uchumi wa wananchi wetu na hivyo kuleta mzigo mzito kwa taifa letu la Tanzania. Utafiti wa sasa wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ume baini ongezeko la hali joto,  pia ongezeko la tofauti za mienendo ya mvua na hasa upungufu wa rasilimali maji kwa upande mmoja na ongezeko la ukame kwa upande wa pili na hata mtungo wa uoto wa asili umeanza kuathiri maisha ya viumbe hai mbalimbali na kutishia uhai wa viumbe hivyo.

Ndugu wageni waalikwa,

Mabadiliko katika mifumo ya pepo duniani, yana athiri pamoja na mambo mengine kupwa na kujaa kwa maji na pengine kusababisha mvua kubwa zisizo za msimu na madhara kwa watu waishio visiwani kama vile ndugu zetu wa Visiwa vya Unguja na Pemba.  Hivi karibuni, mafuriko makubwa yameathiri maisha ya watu pamoja na mali zao katika Jiji la Dar es Salaam, Wilaya za Kilombero, Kilosa, Same na baadhi za Wilaya za Mkoa wa Shinyanga, na maeneo mengine Tanzania.

Ndugu wageni waalikwa,

Mabadiliko haya vilevile yanahusishwa kwa ukaribu na matetemeko katika kanda zenye mabonde ya ufa na milipuko ya volcano kama vile Mlima wa Oldonyo-Lengai uliopo katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.  Ongezeko hili la mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa kiasi kikubwa sasa linaathiri njia mbalimbali za usafiri wa anga na wa majini na zaidi sana linaendelea kuathiri njia na mikakati muhimu ambayo wanajamii wanatumia katika kujikimu kimaisha. Mambo haya kwa ujumla sasa yanaanza kuathiri uhakika wa chakula kwa wanajamii wa makonde yote ya dunia na hasa mataifa maskini duniani.

Ndugu wageni waalikwa,

Ili kukabiliana na mabadiliko haya, Serikali ya Tanzania kupitia  Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira wameandaa mkakati wa kupambana na mabadiliko ya Hali ya hewa na tabianchi wa mwaka 2012 (National Climate Change Strategy) mkakati ambao unaainisha vipaumbele, malengo na namna Taifa letu litakavyojongea mbele katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Katika hili, Taifa lina wahimiza washirika wake mbalimbali kusaidiana na Serikali na Taasisi zake katika kupambana na athari za mabadiliko haya ya hali ya hewa na tabianchi katika ngazi zote.

Ndugu Wageni waalikwa

Kwa kuzingatia wito huu wa Serikali wa  kupambana na kasi ya mabadiliko haya ya hali ya hewa na tabianchi, Ofisi ya Rais  TAMISEMI,  Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Fedha na Mipango  na washirika wetu wa Maendeleo hususan Shirika la Kimataifa la Mazingira na Maendeleo (IIED), Haki Kazi Catalyst (HKC), Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF)  kwa msaada wa kiufundi na  rasilimali fedha kutoka kwa wenzetu wa Serikali ya Uingereza (UK-AID) na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNCDF LoCAL) tumeanzisha mradi wa “Decentralised Climate Finance in Tanzania”  ambao tunauzindua leo wenye lengo la kuhamasisha, kujenga uwezo na kufungua mianya ya kupata fedha zitakazosaidia wananchi wa Tanzania kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2016–2021), ambapo kutakuwa na awamu mbili za utekelezaji; yaani 2016–2018 na 2018-2021. Katika awamu ya kwanza, mradi umelenga kuijengea uwezo wa  OR–TAMISEMI katika maeneo makubwa mawili ambayo ni; (i) uimarishaji wa Taasisi katika uratibu wa mradi na  (ii) uwezo wa kutafuta rasilimali fedha  kwa ajili ya kuziwezesha Mamlaka  za Serikali za Mitaa hapa nchini kuwa na uwezo wa kuziwezesha jamii kuibua na kutekeleza miradi ya  kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Ndugu wageni waalikwa,

Ni matumaini yangu kuwa Halmashauri zote zilizoainishwa kunufaika na mradi huu zitatumia fursa waliyoipata kwa umakini mkubwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Taarifa zinaonesha kuwa kuongezeka kwa Halmashauri tatu za majaribio hadi kufikia 15 kumetokana na kazi nzuri iliyofanywa na Halmashauri 3 za Longido, Ngorongoro na Monduli katika Mradi wa majaribio. Nitoe wito kwa mara nyingine, utendaji wetu uwe na lengo la kutoa matokeo bora zaidi ili kuinusuru jamii na kujenga imani kwa  wafadhili wetu. Kwa kufanya hivyo, wadau hawa hawa na wengine wengi watajitokeza ili mradi kama huu utekelezwe nchi nzima kwani athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi tumeendelea kuzishuhudia sehemu nyingi katika nchi yetu. Uadilifu, utendaji uliotukuka na kujituma utatuvusha hapa tulipo.

Ndugu wageni waalikwa,

Ni matumaini yangu kuwa wanajamii wakisaidiwa na uongozi wa wilaya zetu, watajituma vyema na kujiwajibisha katika kuanzisha, kusimamia na kutekeleza miradi shirikishi na kuvutia fedha zaidi na kupanua wigo wa miradi hiyo kufuatia mifano mizuri iliyokwishaoneshwa na Halmashauri za Wilaya  tatu zilizokuwa katika programu ya majaribio. Halmashauri hizo ni zile za Longido, Monduli na Ngorongoro. Kufuatia matokeo mazuri yaliyokwishaonekana katika Halmashauri za majaribio, mradi huu sasa utapanuka kufikia Halmashauri 15 ambazo ni Kondoa, Manyoni, Bahi, Mpwapwa, Kiteto, Same, Simanjiro, Kilwa, Siha, Mbulu, Iramba na Pangani. Ndugu washiriki, bila kuchukua muda wenu zaidi, lengo la hotuba yangu ni kusimika na kuzindua rasmi mradi huu muhimu wa kuleta fedha zitakazotusaidia na kufungua mianya zaidi ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Ndugu Wageni waalikwa

Jukumu langu katika mkutano huu lilikuwa ni kuzindua rasmi mradi huu; lakini kutokana na umuhimu wa masuala ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, na athari ambazo tumeendelea kuzishuhudia; nimelelazimika kuyasema haya yote. Ninayo imani kuwa huu ni mwanzo mzuri wa safari yetu ndefu ya kukabiliana na mabadiliko haya nchi nzima; tunahitaji kujenga utayari wa wananchi wetu.  Tunawahitaji wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya Tanzania ili kutupatia utaalamu na rasilimali fedha ambavyo ndivyo hasa vikwazo vyetu vikuu ili kukabiliana vilivyo na mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi.

Napenda  kutoa rai kuwa twendeni  tukafanye kazi kwa mtazamo mpya wa kukabiliana na changamoto hizi na kila mmoja wetu akatimize wajibu wake.

Kwa niaba ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kutamka rasmi kuwa mradi huu sasa umezinduliwa rasmi.  Milango yetu sasa ipo wazi kwa washirika wenza kufanya kazi na Serikali ili  kufikia malengo tuliojiwekea.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI KAZI HII

Relevance: 
Undefined